mardi 19 mars 2013

Dar Es Salaam : - Kavumbagu Didier ashtumiwa kushuka kwa kiwango cha soccer na Uongozi wa YANGA...



Uongozi wa Yanga, umejiridhisha kushuka kwa kiwango cha mshambuliaji wake wa kimataifa wa Burundi, Didier Kavumbangu kumetokana na mchezaji huyo kuendekeza anasa kupita kiasi... Kiongozi mmoja wa Yanga, aliyezungumza kwenye vyombo vya habari mapema leo asubuhi jijini hapa Dar es Salaam, bila kutaka kutajwa jina lake, alisema kwamba Kavumbangu amelewa mafanikio aliyoanza nayo katika klabu hiyo na kuangukia kuwa ''muumini'' wa anasa kiasi cha kushusha kiwango chake... Kiongozi huyo alisema hivi, hapa namnukuu: ''Kwa kweli hii hali inasikitisha sana, Kavumbangu amekuwa mtu wa anasa, ile nidhamu aliyokuwa nayo wakati anaingia hapa, haipo tena... Amekuwa mtu fulani kiburi kidogo... Nadhani hii imetokana na mafanikio aliyoanza nayo hapa, alifanya vizuri mzunguko wa kwanza, lakini anasahau kwamba ile ilitokana na juhudi zake mazoezini, akawa fiti akawa anaweza kufanya vizuri''...

Alipo ulizwa kama wamejaribu kuzungumza naye mchezaji huyo, kiongozi huyo alisema: ''Tunazungumza naye sana... Mimi leo hii nimetoka kuzungumza naye, yeye anasema anasingiziwa, wakati watu wanamuona wanatupigia simu na tunakwenda kuthibitisha... Amekuwa mtu wa dansi, pombe, wanawake, hadi anaimbwa kwenye mabendi ya Kikongo... Tazama alivyocheza mechi na Ruvu, yaani alikuwa hawezi hata kutuliza mpira, akiguswa kidogo anaanguka, sasa pale utasema analogwa? Mwili wake hauko vizuri na akili yake haipo uwanjani''... Alipo ulizwa kuhusu mustakabali wa mshambuliaji huyo, kiongozi huyo alisema: '''Inaumiza kichwa, ila kama hatabadilika kwa kipindi kilichobaki kuelekea kumaliza msimu, tutamuuza au tutamtoa kwa mkopo, ili tusajili mtu mwingine, maana kwa sasa hana msaada katika timu...

1 commentaire: