Baadhi ya picha za leo uwanjani :
Tukinukulu jarida la irib redio ikiwa inaskika live kwenye internet wamechapisha habari kuwa :
Kifo cha rais wa zamani wa Afrika Kusini Nelson Mandela kimetoa fursa kwa walimwengu kumuenzi kwa sauti moja shujaa huyo wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi na kusema mengi aliyofanya katika kupigania uhuru na heshima ya wazalendo wa Afrika Kusini. Hata hivyo kati ya matamshi yote yaliyotolewa kuhusu shakshia ya Mandela, maneno yaliyotolewa na viongozi wa nchi ambazo miaka ya huko nyuma zilikuwa waitifaki wakubwa wa utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini, yanatoa mguso maalumu. Kwa mfano tu, Rais Barack Obama wa Marekani amesema Mandela alimpa ilhamu katika maisha yake yeye, huku Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron akisema dunia imempoteza shujaa mkubwa si wa kipindi hiki bali nyakati zote.
Mandela ambaye kifo chake kimesababisha majonzi na simanzi kwa mamilioni ya watu kote duniani, alifungwa jela 27 katika jela ya utawala ambao ulikuwa ukiungwa mkono kwa hali na mali na Marekani na nchi za Ulaya. Tunapoangalia kwa haraka historia ya Afrika Kusini tunabainikiwa kwamba, iwapo viongozi wa utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini wasingepata misaada na uungaji mkono wa kigeni, kamwe wasingeweza kuwatawala wazalendo waliokuwa na hasira wa nchi hiyo. Kwa maneno mengine ni kuwa utawala wa ubaguzi wa rangi wa Afrika Kusini ulisimama na kupata nguvu zaidi kwa sababu ulikuwa ukilinda maslahi ya kiuchumi ya wazungu waliowachache na makampuni makubwa ya Ulaya na Marekani dhidi ya matakwa ya wazalendo. Suala hili ndilo lilikuwa sababu ya kudumu na kuendelea kuwapo madarakani utawala wa Apartheid kwa kipindi cha miongo kadhaa licha ya kukanyaga na kukiuka haki za kimsingi za binadamu na kuamiliana na Waafrika kama wanyama. Viongozi wa utawala wa Apartheid waliokuwa wakijiona bora kuliko wazalendo Waafrika, walifaidika sana na misaada na uungaji mkono mkubwa wa nchi za Magharibi kama Uingereza na Marekani, katika siasa zao hizo chafu na za kishetani. Walitumia uungaji mkono na misaada hiyo ya Magharibi kumfunga jela miaka 27 shujaa Nelson Mandela na kuwaua kinyama maelfu ya wazalendo waliokuwa wakidai haki zao za kimsingi. Katika kipindi chote ambapo Mzee Nelson Mandela alikuwa akitumikia kifungo katika kisiwa cha Robben na kulazimishwa kufanya kazi ngumu, viongozi wa ngazi za juu wa utawala wa kibaguzi walikuwa wakifanya safari katika miji mikuu ya Ulaya na Marekani na kupeana mikono na kugonga bilauri na viongozi wa nchi hiyo. Utawala huo wa kibaguzi uliendelea kukandamiza wananchi wa Afrika Kusini kwa msaada na uungaji mkono wa nchi za Magharibi licha ya malalamiko ya walimwengu dhidi ya jinai zilizokuwa zikifanywa na utawala huo. Utawala huo wa kibaguzi ulianza kudhoofika na hatimaye kusambaratika baada ya nchi za Magharibi kushindwa kustahamili vishindo vya wanapambano shupavu wakiongozwa na Mandela na mashinikizo ya watu katika pembe mbalimbali duniani. Pamoja na hayo na licha ya kuwa Ulaya na Marekani zililazimika kukubali matakwa na wazalendo wa Afrika Kusini hapo mwaka 1990 ambapo utawala wa kibaguzi ulisambaratika, lakini Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani iliendelewa kuliweka jina la shujaa Nelson Mandela katika orodha ya magaidi dunia. Marekani iliendelea kuliweka jina la Mzee Mandela kwenye orodha ya magaidi kwa kipindi cha miaka 15 baada ya Afrika Kusini kupata uhuru. Suala hilo peke yake linaonesha unafiki wa nchi za Magharibi na linafichua maana ya ugaidi katika kamusi za kisiasa za Marekani na waitifaki wake.
Aucun commentaire:
Enregistrer un commentaire