Shujaa wa Afrika na mwanamapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi, Mzee Nelson Mandela amezikwa kitaifa leo kijijini kwake, Qunu, mkoani Cape Mashariki huko Afrika Kusini.
Mazishi ya leo ya Mandela yamehitimisha siku 10 za shughuli ya maziko ambazo ziliwakusanya pamoja mamia ya viongozi wa nchi za dunia huko Afrika Kusini. Karibu wageni waalikwa 4,500 wakiwemo viongozi vigogo, wameshiriki kwenye mazishi hayo ya kitaifa ambayo watu wa kawaida hawakupewa ruhusa ya kushiriki kutokana na familia ya Mandela kusisitiza kuwa suala hilo ni la kifamilia.
Katika hotuba yake kwenye maziko hayo, Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini amesema kuwa wataendeleza urithi ulioachwa na Mandela. Ijapokuwa Mzee Nelson Mandela alizidiwa na ugonjwa kwa muda wa miezi kadhaa, lakini taarifa ya kifo chake iliushitua ulimwengu mzima na hasa wananchi wa Afrika Kusini.
Baada ya kutoka kifungoni, Mandela alichaguliwa kuwa Rais wa Afrika Kusini na kutawala kuanzia mwaka 1994 hadi 1999 alipostaafu ili kuwaachia viongozi wengine kuongoza nchi hiyo.
Amejiwekea sifa nzuri kote ulimwenguni kutokana na mapambano yake ya miaka mingi ya ubaguzi wa rangi na dhulma duniani, na alikuwa mstari wa mbele katika kuliunga mkono taifa madhlumu la Palestina.
Aucun commentaire:
Enregistrer un commentaire