NYASI za Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam zinatarajiwa kuwaka moto Jumapili kwa mpambano wa watani wa jadi katika soka ya Tanzania, Simba na Yanga. Huo utakuwa mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.Yanga SC wana nafasi ya kushinda mchezo huo kwa sababu ni timu iliyokaa pamoja muda mrefu.
Wangapi bado wapo kati ya waliocheza mechi dhidi ya Simba SC Mei 6, mwaka jana Yanga ikifungwa 5-0 na Simba SC?
Langoni alianza Yaw Berko, akampisha Said Mohamed, kulia Nsajigwa Shadrack akampisha Godfrey Taita, kushoto alianza Oscar Joshua, wakati Athumani Iddi ‘Chuji’ alicheza beki ya kati pamoja na Nadir Haroub ‘Cannavaro’, huku Juma Seif ‘Kijiko’ akicheza kama kiungo mkabaji, Nurdin Bakari alicheza kulia, Haruna Niyonzima akazungusha dimba kubwa, mshambuliaji wa kwanza alikuwa Davies Mwape ambaye alimpisha Kenneth Asamoah, Rashid Gumbo alichezeshwa kama mshambuliaji wa pili na kushoto alikuwapo Hamisi Kiiza.
Kati ya wachezaji 14 waliounda kikosi cha kwanza cha Yanga Mei 6, mwaka jana tu waliobaki ni watano tu na kati ya hao, ni wanne tu ambao bado wana nafasi katika kikosi cha kwanza, Chuji, Cannavaro, Niyonzima na Kiiza, wakati Oscar Joshua tayari amemuachia nafasi David Luhende. Je, bado unaweza kuendelea kusema Yanga ni timu iliyokaa pamoja muda mrefu, ikiwa kutoka kikosi cha kwanza cha Mei mwaka jana wamebaki wachezaji wanne tu?
Kikosi cha sasa cha Yanga SC, waliobaki kutoka kikosi cha Mei mwaka jana ni Kiiza, Chuji, Niyonzima na Cannavaro pekee |
Ukizungumzia wazoefu waliosajiliwa kutoka nje ya nchi kama Didier Kavumbangu na Mbuyu Twite, pia Simba SC imesajili Abbel Dhaira, Kaze Gilbert, Amisi Tambwe pamoja na kuwarejesha Joseph Owino, Abdulhalim Humud, Henry Joseph na Ramadhani Chombo ‘Redondo’.
Huwezi kuona dhana kwamba Yanga imekaa muda mrefu kuliko Simba SC na ndiyo maana inapewa nafasi ya kuifunga SImba SC inatoka wapi. Simon Msuva na Frank Domayo hawana tofauti na akina Jonas Mkude na Edward Christopher ni jinsi ya kuwatumia tu.
Kitu ambacho kinaonekana katika Yanga SC kwa sasa ni kwamba wanajiamini kutokana na kwamba wao ni mabingwa wa nchi na ndiyo walioshinda mchezo wa mwisho timu hizo zilipokutana, lakini pia wako vizuri kiuchumi chini ya
Didier Kavumbangu hakuwepo Mei mwaka jana
Mwenyekiti wao, Yussuf Manji na mamilionea wengine, akina Seif Magari, Abdallah Bin Kleb na Mussa Katabaro.
Lakini pamoja na hayo, Simba SC hawawezi kuwa wanyonge sana wakikumbuka kipigo cha mbwa mwizi walichompa mtani Mei 6, mwaka jana Uwanja wa Taifa cha 5-0, Wekundu wa Msimbazi, Simba SC walipokabidhiwa Kombe lao la ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania kwa shangwe nzito.
Mabao ya Simba yalifungwa na Emmanuel Okwi mawili, Juma Kaseja, Felix Sunzu na Patrick Mutesa Mafisango.
Hicho kilikuwa kipigo cha pili kikali kihistoria Simba wanaifunga Yanga, baada ya zile 6-0 za mwaka 1977.
Ilikuwa ni hoi hoi, nderemo na vifijo kuanzia Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam hadi kona mbalimbali za Jiji, rangi nyekundu na nyeupe zikiwa zimetawala na shangwe za Simba.
Hadi mapumziko, Simba walikuwa tayari mbele kwa bao 1-0, lililofungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Arnold Okwi dakika ya pili tu ya mchezo huo.
Okwi alimtungua kipa Mghana, Yaw Berko baada ya kutumia mwanya wa kuzubaa kwa mabeki wa Yanga mwanzoni mwa mchezo huo.
Katika kipindi hicho, Okwi alikuwa akimpita kwa urahisi beki mkongwe wa Yanga, Nsajigwa Shadrack Joel Mwandemele ambaye aliishia kumkwatua mara kwa mara, jambo ambalo lilimponza kwenda chumba cha kupumzikia akiwa ana kadi moja ya njano aliyopewa dakika ya 39.
Pamoja na kufungwa bao hilo, Yanga waliendelea kucheza kwa utulivu, wakigongeana pasi vizuri na kutengeneza nafasi kadhaa, ingawa kikwazo kilikuwa Tanzania One, Juma kaseja.
Nafasi pekee nzuri katika kipindi hicho na ambayo Yanga wataijutia waliipata dakika ya 35, baada ya Mwanasoka Bora wa Uganda, Hamisi Kiiza kuwatoka vizuri mabeki wa Simba, lakini akiwa amebaki yeye na kipa, hesabu zake ziliendana na Kaseja.
Mrisho Ngassa hakuwepo Mei mwaka jana. |
Kipindi cha pili, Yanga walianza kwa mabadiliko, wakimtoa kipa Yaw Berko na kumuingiza Said Mohamed Kasarama, wakati Simba walimpumzisha Mwinyi Kazimoto na nafasi yake kuchukuliwa na Jonas Mkude.
Simba waliingia tena kwa kasi na kufanikiwa kupata mabao matatu ya haraka haraka, mawili yakipitia kwa Nsajigwa.
Bao la pili la Simba lilitokana na penalti, baada ya Nsajigwa Shadrack kumkwatua Okwi kwenye eneo la hatari na Felix Sunzu akaenda kufunga kwa penalti dakika ya 56.
Okwi alifunga bao la tatu dakika ya 62, baada ya kumtoka Nsajigwa Fusso na kumchambua kipa Said Mohamed Kasarama.
Baada ya bao hilo, kocha Fred Felix Minziro alipumzishwa Nsajigwa na kumuingiza Godfrey Taita Magina.
Dakika ya 67 Uhuru Suleiman aliangushwa na Taita kwenye eneo la hatari na Juma Kaseja akaenda kufunga bao la nne kwa penalti. Patrick Mafisango (sasa marehemu) alifunga bao la tano kwa penalti pia dakika ya 72.
Katika mchezo huo, kikosi cha Simba SC kilikuwa; Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah, Shomary Kapombe, Kelvin Yondan, Patrick Mafisango/Obadia Mungusa, Uhuru Suleiman, Mwinyi Kazimoto/Jonas Mkude, Felix Sunzu/Edward Christopher, Haruna Moshi ‘Boban’ na Emmanuel Okwi.
Yanga: Yaw Berko/Said Mohamed, Nsajigwa Shadrack/Godfrey Taita, Oscar Joshua, Athumani Iddi ‘Chuji’, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Juma Seif ‘Kijiko’, Nurdin Bakari, Haruna Niyonzima, Davies Mwape/Kenneth Asamoah, Rashid Gumbo na Hamisi Kiiza.
Naam, hivi ndivyo mambo yalivyokuwa Mei 6, 2012 na baada ya hapo Yanga wakafanya mabadiliko makubwa ya uongozi, wakimtoa Mwenyekiti wao wa wakati huo, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga na kuweka safu mpya ya uongozi, chini ya Mwenyekiti Yussuf Manji, ambaye alianza na sare ya 1-1 Oktoba 3, mwaka jana dhidi ya watani na baadaye kushinda 2-0 Mei 18, mwaka huu.
Je, Jumapili tutarajie nini Uwanja wa Taifa, miamba hiyo ikikutana tena? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona.
VIPIGO VINGINE VYA ‘MBWA MWIZI’ SIMBA WALIVYOICHAPA YANGA:
LIGI KUU BARA:
JULAI 19, 1977
Simba v Yanga
6-0
WAFUNGAJI:
Abdallah Kibadeni dk. 10, 42 na 89, Jumanne Hassan 'Masimenti' dk. 60 na 73, Selemani Sanga alijifunga dk. 20.
JULAI 2, 1994
Simba v Yanga
4-1
WAFUNGAJI:
Simba: George Masatu, Athumani China, Madaraka Selemani, Dua Saidi Yanga; Constantine Kimanda.
MACHI 31, 2002.
Simba Vs Yanga 4-1 (Kombe la Tusker)
WAFUNGAJI:
SIMBA: Mark Sirengo dk. 3 na 76, Madaraka Selemani dk. 32 na Emanuel Gabriel dk. 83.
YANGA: Sekilojo Chambua dk 16.
(Mechi hii ya fainali iliyohudhuriwa na rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, chupuchupu ivunjike dakika ya 32, baada ya Madaraka kufunga bao ambalo kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Manyika Peter, aliushika mpira kwa makusudi, ili kuuweka sawa. Rais wa Yanga wakati huo, Tarimba Abbas aliinuka na kuwaonyesha ishara wachezaji wake watoke uwanjani na hapo ndipo meza kuu aliyokuwa ameketi mzee Mwinyi, ilipoanza kushambuliwa kwa chupa za maji na mashabiki wa Yanga. Mwamuzi wa mchezo huo, Abdulkadir Omar alisubiri hadi vurugu zilipotulizwa na FFU ndipo akaendeleza mchezo. Tarimba alitoka nje na hakutaka kuendelea kushuhudia mchezo huo. Baada ya hapo, alifungiwa na Chama cha Soka Tanzania, FAT).
MEI 6, 2012
Samba 5-0 Yanga SC
WAFUNGAJI:
Emmanuel Okwi (dk 2 na 62), Felix Sunzu (penalti 56), Juma Kaseja (penalti dk 67) na Patrick Mafisango (penalti dk 72)
Aucun commentaire:
Enregistrer un commentaire